Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewaaga wapigakura wake kuwa hatakuwa tena mbunge wao, akisema kuwa kesi ya dhidi ya Chadema ilitupwa na Mahakama Kuu kutokana na baadhi ya majaji kutajwa kwenye kashfa ya escrow.
Chadema ilimvua Zitto uanachama saa chache baada ya Mahakama Kuu kutupa shauri lake alilofungua akitaka chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa nyaraka za mwenendo wa vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote, huku akifanikiwa kupata amri ya muda ya kuizuia Chadema kumjadili.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mwandiga mkoani Kigoma jana, Zitto alisema hatakuwa mbunge wa jimbo hilo baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, na akatumia fursa hiyo kueleza safari yake ya kisiasa ndani ya Chadema na mtazamo wake baada ya kufukuzwa uanachama.
“Nimejifunza mengi nikiwa mbunge. Katika utumishi wangu kwenu, bungeni nimejifunza namna nchi yetu inavyoendeshwa. Katika kujifunza huko kuna mambo kadhaa nimefanya ya kujivunia na mengine ni makosa,” alisema Zitto ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa Chadema.
“Nimejifunza kuwa mzalendo zaidi kwa nchi yangu na kuwatumikia watu wa nchi hii. Ndiyo maana hamkunisikia tu nikitetea watu wa Kigoma pekee, bali watu maeneo mengine ya nchi yetu na makundi mbalimbali ya kijamii.”
Alisema safari yake ya ubunge ilikuwa ngumu yenye mafunzo makubwa na imemfanya apevuke kifikra na kupata mafunzo.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Zitto alisema: “Bado nina nia ya dhati ya kuendelea kuwatumika Watanzania kama mwakilishi wao kupitia jimbo lolote nchini.
Nitaendelea kuwapo kwa uwezo wa Mungu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. Itakuwa kwa tiketi gani na jukwaa gani watu watayajua hayo wiki hii.”
Akizungumzia sakata la escrow lililowahusisha watendaji mbalimbali wa Serikali, wakiwamo majaji na hukumu ya kesi yake, Zitto alirudia tena kauli yake kuwa hukumu hiyo imetolewa bila yeye kujua. “Kwa kazi ninazozifanya kuna miguu ya watu wengi ninayoikanyaga.
Moja ya ninaowakanyaga ni mahakama. Kuna majaji ambao taarifa ya kamati ya PAC imewataja kuhusika na escrow na wanatakiwa kuchunguzwa,” alisema.
Alisema inawezekana ndani ya mahakama wameona hukumu ya kesi hiyo ndiyo eneo zuri la kumkomoa.
“Inawezekana pia watu ambao kupitia kazi za PAC, nimesababisha wachukuliwe hatua nao pia wanaweza kuwa wameshiriki kwa njia moja au nyingine. Lakini pia inawezekana ni taratibu za kawaida za mahakama. Mpaka hukumu inatolewa kuna maswali mengi hayana majibu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment