Takribani miezi mitatu na ushei tangu sakata la uchotwaji wa fedha zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow kutikisa nchi huku mawaziri wawili na mwanasheria mkuu wa serikali wakiondoka madarakani na katibu mkuu mmoja akichunguzwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amefichua kuwa wajumbe wote wa kamati hiyo wataadhibiwa vibaya kwenye majimbo yao kama njia ya kulipiza kisasi kutokana na kuwaumbua wote walionufaika na fedha hizo.
Katika mahojiano na kituo cha ITV kwenye kipindi cha Dakika 45, kilichorushwa jana usiku, Zitto amesema kuwa wakati PAC wakiendelea kuchambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) juu ya Escrow, mjumbe mmoja wa kamati hiyo aliitwa na ‘wakubwa’na kuelezwa kwamba akifika bungeni awageuke wenzake na aseme kuwa mgogoro wa ripoti ya Escrow iliandikwa kwa shinikizo la mfanyabiashara mmoja.
“Mmoja wa wajumbe wangu aliitwa kuombwa aingie bungeni aseme kwamba kuna mfanyabiashara mmoja mkubwa amewapa wajumbe wa PAC fedha ili watengeneze hiyo ripoti ya PAC,” alisema.
Aliongeza kuwa mjumbe huyo alipokataa aliambiwa: “ Umekataa kutekeleza hili? Sasa tumetenga Sh. milioni 500 kwa kila jimbo kwa kila mjumbe wa PAC ili kuhakikisha hawarudi bungeni.”
Hata hivyo, Zitto hakutaka kumtaja mfanyabiashara huyo.
Zitto alifafanua kwamba maana ya fedha hizo ni kwamba watu hao watatafuta wagombea wa kupambana na waliokuwa wajumbe wa PAC kwa nguvu ya fedha ili wahakikishe wanakwama kutetea majimbo yao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aliongeza kuwa kitendo cha kutaja wanufaika wa Escrow wazi wazi, kama vile majaji, mawaziri na wengine wote alijua kuwa hawawezi kukubali jambo hilo lipite hivi hivi tu.
“Kuna watu wana fedha nyingi bwana. Kwa mfano IPTL kwa mwezi wanalipwa capacity charge Sh. bilioni nne,” alisema.
Kwa hiyo, kitakachoendelea kwenye uchaguzi mkuu wajumbe wa PAC watawekewa watu wa kupambana nao kuanzia kwenye kura za maoni, hata wakishinda watawekewa wapinzani katika majimbo yao na fedha nyingi zitatumika kuhakikisha wanaangushwa. Wajumbe walioshirikia uchambuzi wa ripoti ya Escrow ndani ya PAC walikuwa 17.
Wajumbe hao ni Zitto, Deo Filikunjombe, Desderius Mipata, Asha Jecha, Lucy Owenya, Ester Matiko, John Cheyo, Zaynabu Vulu, Ally Keissy, Zainab Kawawa, Kheri Ali Khamis, Faida Mohammed Bakar, Ismail Aden Rage na Modestus Kilufi.
Walioongezwa ni Kangi Lugola, Luhaga Mpina na Dk. Hamisi Kigwangalla.
Hata hivyo, Zitto alisema hadi sasa hana ushahidi kwamba kesi yake dhidi ya Chadema imetupwa mahakamani kwa sababu za Escrow, ingawa anasisitiza kwamba mkakati wa kutengeneza majungu na mambo ya ovyo ovyo dhidi ya wajumbe wa PAC ulianza wakati wa kujadili ripoti yao bungeni mwaka jana.
JE, AMENUFAIKA NA MGAWO WA ESCROW?
Zitto anasema kuwa tuhuma kwamba naye alinufaika na fedha za Escrow hazina msingi wowote na alikwisha kusema kuwa suala hilo lichunguzwe baada ya kuibuliwa maneno ya kuokoteza na kuwasilishwa bungeni.
Alitoboa siri nyingine kwamba usiku wa kuamkia siku ya PAC kuwasilisha ripoti yake kuhusu Escrow bungeni, kila mbunge anakoishi chini ya mlango wake lilipenyezwa kabrasha lililokuwa limejaa habari za kupika, nia ikiwa ni kubadili upepo ili kuonyesha kuwa naye (Zitto) alikuwa amenufaika na fedha hizo.
“Wanadai kwamba eti nami nilimtumia dada mmoja… alikwenda kuomba fedha kwa niaba yangu ili nimuuguze mama yangu,” alisema Zitto na kuongeza kuwa:
“Huu ni uongo tu mama yangu alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, matibabu yake na gharama zote za matibabu yake zilikuwa zinalipwa na Bunge hilo. Sasa mimi niombe hela ya kumtibu wakati gharama zilikuwa zinalipwa zote?”
Chanzo: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment