Siku moja baada ya katibu mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa kuwataka Watanzania wajiandae kwa “Serikali Mpya” aliyodai itapatikana Oktoba 31 baada ya Uchaguzi Mkuu, gazeti la Mwananchi limebaini mkakati wa ushindi unaopangwa na chama hicho cha upinzani.
Hadi sasa, Chadema ndio chama kinachoongoza kwa upande wa upinzani kulingana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita na wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, na inaonekana kujipanga kupaka mafanikio makubwa zaidi mwezi Oktoba.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete alishinda kwa kupata asilimia 61.17, ikiwa ni pungufu ya asilimia 20 ya kura alizopata mwaka 2005, wakati Chadema ilimsimamisha Dk Willbroad Slaa aliyepata asilimia 26.34 akiwa anasimama kwa mara ya kwanza.
Huku CCM ikiwa katika mchakato mgumu wa kumpata mrithi wa Kikwete uliogubikwa na adhabu dhidi ya makada wanaotajwa kutaka nafasi hiyo, Chadema iliweka mkakati wake katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Januari mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari ambazo Mwananchi imezipata, chama hicho kimelenga pamoja na mambo mengine kupeleka madaraka kwenye ngazi ya kanda badala ya mambo yote kutegemewa yafanywe na makao makuu.
Chadema, habari hizo zinasema, imeunda kanda 10 ambazo ni Kanda ya Serengeti, inayoundwa na mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara, Ziwa Victoria (Geita, Mwanza, Kagera), Nyanda za Juu Kusini (Rukwa, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Iringa), Kanda ya Kusini (Lindi na Mtwara).
Nyingine ni Kanda ya Kati (Singida, Dodoma na Morogoro), Kanda ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara), Kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Kanda ya Pwani (Temeke, Ilala na Kinondoni), Kanda ya Unguja(Kusini Unguja, Kaskazini Unguja na Mjini ) na Kanda ya Pemba (Kusini Pemba na Kaskazini Pemba).
Kanda hizo zitawezeshwa kwa mafunzo na kiuchumi ili kuzijengea uwezo wa kushughulikia mambo yake, hasa wakati wa uchaguzi bila ya kutegemea ofisi kuu.
Kwa mujibu wa habari hizo, kanda hizo pia zinazindua vikundi vyake vya ulinzi, ambavyo kazi kubwa inaonekana itakuwa ya kulinda kura ili kukabiliana na tatizo kubwa la upungufu wa rasilimali watu wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Pia kuundwa kwa Mabaraza ya Uongozi ya Kanda kutawezesha mashauri mengi kwenye ngazi ya mikoa kutatuliwa bila ya kutegemea ofisi kuu.
Tayari mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ameshafanya ziara kwenye baadhi ya kanda na kufanya vikao na Mabaraza ya Uongozi ya Kanda kuyashirikisha mikakati hiyo, sambamba na kuzindua vikundi vya ulinzi.
Lakini alipoulizwa kuhusu mpango huo, Mbowe hakutaka kuwa bayana.
0 comments:
Post a Comment