Zitto Kabwe Kutua Leo Kigoma Kuwasilimuliwa Yaliyomkuta Mpaka Kufukuzwa Chadema

Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kumvua uanachama, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe LEo atatua jimboni kwake kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.

Uamuzi wa kumfukuza Zitto (pichani) ulifikiwa juzi ikiwa ni muda mfupi baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi aliyofungua Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini na katibu mkuu wa Chadema, iliyokuwa imeshikilia uanachama wake.

Mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ndiye alitangaza kutimuliwa kwa Zitto akisema ni kutokana na kufungua kesi mahakamani, kinyume na Katiba ya Chadema kipengele cha 8 (a) (x).

Jana, Zitto ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) aliongoza kikao cha kamati hiyo, kilichojadili taarifa ya Tanesco na baadaye alisisitiza kwamba hana taarifa rasmi ya uamuzi wa mahakama na atakapoipata atazungumzia hatima yake.

“Kama mnavyoona mimi naendelea na kazi na wala sina taarifa rasmi lakini nikipata taarifa rasmi na mimi nitatoa taarifa rasmi, Ijumaa (kesho) ninakwenda jimboni kuzungumza na wapigakura wangu ambao niliwaahidi kufanya hivyo kabla ya vikao vya Bunge kuanza Jumanne ijayo,” alisema Zitto ambaye taarifa zinasema alikuwa amepapanga kuwaaga wapiga kura na baadaye kutimkia kwenye chama kipya cha ACT alichokiasisi.

“Muhimu kwangu ni kufanya kazi ya Watanzania na nitafanya kwa mazingira yoyote yale. Siasa yangu inajikita katika masuala, siyo watu, ukiandika kuhusu Zitto siyo kwa ajili ya mtu bali masilahi ya Taifa.

“Nakuzwa, nakomazwa na hii ni changamoto, nitaendelea kufanya kazi zangu hadi nitakapopata taarifa rasmi.”

Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando juzi aliliambia gazeti hili kwamba, anafuatilia uamuzi huo wa mahakama kabla ya kuona ni hatua gani watazichukua.

Chanzo: Mwananchi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment