Habari zinasema, wakati Komba akihaha kuokoa nyumba yake kutokana na tanganzo la benki ya CRDB kwenye vyombo vya habari; huku akiwa tayari ameonekana kukata tamaa; ghafla Jumamosi jioni alipatwa na shinikizo la damu na kufariki dunia.
MBUNGE wa Mbinga Magharibi (CCM), John Komba, amefariki dunia kutokana na kuzongwa na mzigo wa madeni, likiwamo mkopo kutoka Benki ya CRDB.
Benki hiyo ilitoa kiasi cha sh. 12 bilioni kwa mwanasiasa huyo mwaka 2009, lakini hadi mauti yanamkuta, alikuwa hajaweza kulipa deni hilo.
Mamilioni hayo ya shilingi yalitolewa na CRDB Benki kwa mbunge huyo kwa ajili ajili ya kuendeleza shule zake mbili alizokuwa akizimiliki – shule ya Sekondari ya Bakili Muluzi na Shule ya Msingi ya Coletha – zilizoko jijini Dar es Salaam.
Hadi anafariki dunia, Komba alikuwa amebakiza kiasi cha zaidi ya sh. 78.5 milioni. Deni la Benki linatokana na mkopo pamoja na riba ya asilimia 17 katika kipindi cha miaka mitano ya uhai wa mkopo.
Komba amefariki dunia Jumamosi iliyopita, miezi mitatu baada ya Benki ya CRDB kuuza shule zake.
Mbali na kuuza shule, benki iliuza vifaa mbalimbali, likiwamo eneo la ukubwa wa mita za mraba zaidi ya 34,000 lililotumika kutoa mkopo wa sh. 900 milioni mwaka 2009.
Shule za Komba pamoja na vifaa vyake, vimenunuliwa na mfanyabiashara mmoja mmoja.
Gazeti hili limeelezwa kuwa Komba alijaribu, bila mafanikio, kushawishi serikali kununua shule yake; na kwamba alitinga hadi ikulu na makao makuu ya CCM kuomba msaada ili shule na nyumba yake visiuzwe.
Hata hivyo, taarifa zinasema, Komba hakufanikiwa kupata msaada wa kuzuia shule kuuzwa. Hadi anafariki dunia benki ilikuwa inajiandaa kuuza nyumba yake.
“Yule bwana alifika hadi ikulu kuomba msaada ili nyumba yake isiuzwe. Alitaka serikali imsaidie kununua shule yake; au kuomba benki izuie kwa muda uuzaji kwa kuwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lilikuwa limekubali kununua eneo hilo kwa bei ya soko,” ameeleza mtoa taarifa.
Baada ya shule kuuzwa na deni kushindwa kumalizika, mtoa taarifa anasema, Komba alirudi tena ikulu na CCM kuomba msaada wa kukwamua nyumba yake.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alijaribu kunusuru shule ya Komba kupigwa mnada kwa kuiandikia benki ya CRDB kumpa mwanasiasa huyo muda zaidi wa nyongeza ili kulipa deni lake.
Hata hivyo, pamoja na maombi ya Pinda kupewa nafasi, bado Komba alishindwa kulipa deni hilo.
Komba aliyekuwa anajulikana kwa jina maarufu la “Mzee wa kutoa mitaji kwa vimwana,” alizikwa juzi Jumanne, katika jimbo lake la uchaguzi la Mbinga Magharibi.
Credit: Mwanahalisi
0 comments:
Post a Comment