Tundu Lissu Apasua Jipu Jipya Kuhusu Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu jana aliwatoa jasho Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu wa Bunge),  Jenister Mhagama kuhusu kupitishwa kwa Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa akidai kuwa unagusa mambo ya Muungano na kuvunja Katiba ya Nchi.
 Mvutano huo ulisababisha Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kutamka kuwa Lissu ni mwanasheria mzuri lakini kwa hoja hiyo aiache Serikali ishinde, akimaanisha kuwa akubali muswada huo upitishwe.
 Katika hoja yake, Lissu alisema muswada huo una mgongano wa kisheria kuhusu mamlaka ya kuweka utaratibu wa kutangaza maafa na kutangaza hali ya hatari, akisema kuwa sheria hiyo imempora Rais madaraka ya kutangaza maafa na kuyapeleka kwa waziri.
 Masaju na Mhagama walijichanganya na kusababisha wabunge kuangua kicheko huku Lissu kila alipopewa nafasi akisisitiza kuwa haiwezekani waziri amshauri Rais kutangaza maafa.
 Masaju alilazimika kusoma vifungu mbalimbali vya sheria huku akisisitiza kuwa kabla ya kuletwa kwa muswada huo, Serikali ilishauriana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) huku akisoma Ibara ya 32 ya Katiba inayozungumzia Rais kutangaza hali ya hatari.
 Katika hoja yake ya msingi, Lissu alisema, kutokana na muswada huo kugusa mambo ya Muungano ili upitishwe, inatakiwa upigiwe kura na theluthi mbili ya wabunge kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge kutoka Zanzibar.
 Wakichangia hoja ya Lissu, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali waliungana na Lissu kupinga vifungu vya muswada huo. Hata hivyo, muswada huo haukupitishwa kutokana na akidi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment