Lowassa Amemjibu Nape Kuwa Hawezi Kuzuia Mafuriko kwa Mikono.

Siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kusema Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, anaweza kupoteza sifa za kuwania urais kutokana na makundi ya jamii yanayomiminika nyumbani kwake kumshawishi awanie nafasi hiyo, Lowassa amemjibu na kusema hawezi kuzuia mafuriko kwa mikono.
Kadhalika, Lowassa amesema mambo ya Chama hayajadiliwi mtaani (kwenye vyombo vya habari), bali malalamiko yoyote yanapelekwa kwenye vikao halali vya CCM, yanajadiliwa na kutolewa uamuzi kwa mujibu wa kanuni na taratibu.
Hata hivyo, amewataka wafuasi wake pamoja na makundi mbalimbali ambayo yalikuwa yamejiandaa kwenda nyumbani kwake kumshawishi, wasitishe kwanza safari yao hadi hapo Chama kitakapotoa maelekezo ya ‘namna ya kushawishi.’
Lowassa aliyasema hayo nyumbani kwake jana, alipokuwa akipokea ujumbe wa waendesha bodaboda 60 kutoka Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya ambao walikwenda kumshawishi awanie urais muda utakapofika.
Alisema kwa kanuni na taratibu za CCM, mambo ya chama humalizwa kwenye vikao vya chama, kwa kuzungumza hadi kuelewana na kufikia muafaka, lakini siyo kwenye vyombo vya habari.
“Mambo ya Chama hayawezi kuzungumzwa kwenye vyombo vya habari kwenye tv, redio; mara huyu hivi, huyu hivi, mkiona chama kinakwenda kwenye utaratibu huo ni hatari sana…CCM ninayoijua mimi ni ya vikao, kwa hiyo sikusudii kujibu hizo hoja, kwanza rafiki yangu Bashe (Hussein), amezieleza vizuri sana, lakini sikusudii kusema zaidi ya hayo yaliyosemwa na Bashe,” alisema.
Alisema anashangaa kuona watu wakizusha kwamba watu wanaokuja nyumbani kwake kumshawishi amewaita na kuwalipa jambo ambalo ni uongo kwa kuwa hana fedha za kulipa watu wengi wanaokuja kwake na hana pia uwezo wa kuwapikia chakula.
“Wanasema mnakuja nimewaiteni ninawapa fedha, hela za kuwapa ninazitoa wapi, mkija hapa nikiwawekea maturubai ni kosa, mkiwa na viti ni makosa na wanasema nawapikieni chakula. Mambo ya ajabu sana, yanasemwa na watu wazima watu wenye heshima zao; juzi kulikuwa na vijana 300 hapa, nitawapikia chakula nitaweza wapi, ni vibaya sana kumdhalilisha mwenzako kwamba maisha yake yote akili yake ni kufikiria tumbo, huyu hana cha kufikiri isipokuwa tumbo,” alisema Lowassa.
“Nimewahi kuja huko Mbarali kuwashawishi mje kwangu? Au nimewapeni   hela   leo   mlipokuja hapa, hata soda zenyewe hamjanywa,” alisema Lowassa huku vijana wakisema hawajashawishiwa naye.
Aliongeza: “Yananisikitisha sana maneno hayo, lakini hayanikatishi tamaa nitaendelea kama ilivyo kawaida. Nawahakikishie nimeyasikia maneno hayo, lakini najua maneno mazuri huwa yanazungumzwa kwenye chama, nategemea yatajadiliwa kwenye vikao vya chama.”
Lowassa alisema: “Na utaratibu huu ulioanza na watu, (kuja nyumbani kwake), mimi ni vigumu kuuzuia. Mimi ni vigumu kuzuia mafuriko kwa mikono. Mafuriko yanakuja mimi nayazuia kwa mikono, nitaweza kweli?”
“Ila nashauri tufanye hivi, wengine ambao hawajaja wanisikilize, hebu tusubiri Chama kitoe maelekezo, kama wamesema hii inatafsiriwa kwamba ni kampeni, tungoje basi wasema tufanye nini watu wanaotaka kuja kushawishi,” alisema.
Alisema watu wanaokwenda kumshawishi wanatii maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, ambayo aliyatoa mjini Songea wakati wa sherehe za miaka 38 ya CCM, aliposema kwamba wanachama wanaweza kumshawishi mgombea wanayeona anafaa.
“Na mimi nilikuwapo kiwanjani pale akasema mkiona hao waliopo hawatoshi, bado muda upo washawishini wengine waingie. Sasa mkifanya hivi ni kosa, ni kampeni, ipi ni kampeni na ipi siyo kampeni?,” alisema na kuhoji.
“Kwa hiyo nawashauri wale ambao hawajaja, tusiingize mgogoro kwenye Chama, tungoje tupate maelekezo, mimi ninahakika tutapata nafasi, jambo moja ninahakika na ninataka kuwapa matumaini ipo siku Watanzania watapata uhuru wa kusema juu ya mtu mimi, iko siku watapiga kura zao kusema naam ama hapana kwa hiyo tungojee hiyo siku.”
Alisema anatambua Watanzania wengi wanampenda kwa kazi zake alizofanya akiwa kwenye ngazi mbalimbali serikalini na kutaka wanaomshambulia wasubiri Watanzania wenyewe waamue kwenye sanduku la kura.
“Ninahakika wapo Watanzania wengi wanaonipenda kama walivyosema kwa kazi zangu, watapata nafasi ya kusema naam ama hapana, kwa hiyo huyo anayepiga kelele nyingi sijui nitoke kwenye chama sijui nifanye kitu gani angoje wanaCCM na Watanzania waamue. Mimi ni mwanademokrasia naamini kwenye demokrasi, lakini naamini kwenye utendaji bora, kama mlioufanya leo wa kutembea kilometa 600 kutoka Mbarali kuja kunitembelea hapa ni kazi kubwa ya utashi mkubwa sana, ni watu wanaojitolea, wanaojiamini, na mimi ninaamini Watanzania wengi wanaoniamini kwa mambo ambayo nimeyafanya,” alisema.
Aliwasihi vijana hao kupuuza taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari jana na kuwaomba waendelee kukiunga mkono chama hicho.
Alisema safari ya vijana hao kusafiri kilimita 600 kwa bodaboda kutoka Mbarali imemtia moyo na haya kwa kuweka wazi mambo wanayoyaamini.
Alisema vijana wa bodaboda wanafanya kazi kubwa nchini ikiwamo ulinzi na usalama hivyo ni kundi linalohitaji kuendelea kusaidiwa.
“Mimi nitaendelea kushirikiana nao siku zote katika nafasi yoyote nitakayokuwa nayo. Mmekuja siku mbaya kidogo kwa sababu jana kuna watu wamesema kwenye vyombo vya habari maneno mengi ambayo kwa malezi yangu mimi mambo ya chama humalizwa kwenye vikao siyo kwenye vyombo vya habari, lakini yasiwakatishe tama,” alisema.
Awali, Kamanda wa Vijana wa CCM wilayani Mbarali, Ibrahim Mwakabwanga, alisema Lowassa hana uwezo wa kushawishi kila kundi na hata wao wamejikusanya wenyewe, wamejigharimia na wameacha shughuli zao na kuamua kuja Dodoma kumshawishi kwa kuwa wanaona ndiye kiongozi ndani ya CCM anayefaa kwa sasa.
Chanzo: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment