Viongozi Watatu Chadema Sasa Wapata Dhamana.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imewaachia kwa dhamana viongozi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Diwani wa Kata ya Ubungo, Boniface Jacob (32) wanaokabiliwa na mashtaka mawili ya kuteka na kujeruhi.

Mbali na Jacob, washitakiwa wengine ni Mkuu wa Walinzi, Hemed Sabula (48) na Ofisa Utawala wa chama hicho, Benson Mramba (30).

Wote waliachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

Walifikishwa mahakamani wakituhumiwa kumteka aliyekuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, Khalid Kagenzi.

Jana saa 3:00 asubuhi washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza dhamana.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka dhidi yao wiki iliyopita mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanadaiwa kuwa Machi 7, mwaka huu, walimjeruhi na kumteka nyara Kagenzi kwa nia ya kuzuia uhuru wake.

Wakili wa Serikali, Janeth Kitale, alidai washtakiwa hao walifanya makosa hayo kinyume cha kifungu cha 225 na 249 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Pia alidai kuwa Machi 7, mwaka huu, washitakiwa hao kwa pamoja wakiwa katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, walimjeruhi Kangezi maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Wakili huyo aliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao kwa pamoja, wakiwa katika ofisi hizo za Chadema, walimteka Kagenzi na kumpeleka Hoteli ya River View, iliyopo Sinza.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment