Jaji Lubuva: Hakuna Kura ya Maoni Bila Uandikishaji BVR Kukamilika

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (Nec), Jaji mstaafu Damian Lubuva amesisitiza kuwa Kura ya Maoni kwa Katiba Inayopendekezwa haitafanyika mpaka uandikishaji watu katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kupitia mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) ukamilike.
Jaji Lubuva alisema hayo juzi katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake, kwamba kwa sasa, Daftari la Kudumu ndiyo kazi namba moja ndipo yafuate matukio ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu.
Katika msisitizo wake, Jaji Luvuba amewataka Watanzania kuondoa hofu kwamba Kura ya Maoni huenda isifanyike Aprili 30, mwaka huu kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete badala yake waweke imani kuwa tume hiyo itajitahidi kukamilisha uandikishaji ndani ya muda uliopangwa.
“Tarehe ile haijabadilishwa, iko palepale na siku zote nimekuwa nikisema kuwa tutakamilisha ndani ya muda uliopangwa. Pia ikifika tarehe ya mwisho bado hatujakamilisha shughuli hii tutawaambia,” alisema Jaji Lubuva.
“Sisi tume hatutafanya Kura ya Maoni kama daftari halijakamilika. Ndiyo kwanza tumeanza Njombe na baadaye tutaenda mikoa mingine tutakayotangaza hapo baadaye; tukishindwa nitasema ile kazi yetu namba moja ya uandikishaji sijakamilisha,” aliongeza.
Alisema wanaongeza kasi ya uandikishaji mkoani Njombe, ambapo kuanzia leo kutakuwa na mashine zote 250 za BVR zilizonunuliwa awali kwa ajili ya majaribio katika baadhi ya majimbo matatu katika mikoa ya Dar es Salaam, Katavi na Morogoro.
Kwa nyakati tofauti wadau mbalimbali wa uchaguzi wameonyesha wasiwasi kuwa huenda tume hiyo isikamilishe uandikishaji wapigakura ndani ya muda uliopangwa kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji na uchache wa mashine za BVR.
Jaji Lubuva alisema kuwa Serikali imefanya malipo ya ununuzi wa mashine 7,750 hivi majuzi na kwamba kulingana na mchakato huo kuchelewa na uingizaji nao umechelewa.
Kutokana na kuchelewa huko, mashine hizo zitaingia ndani ya wiki mbili zijazo. Awali, Nec ilitarajia mashine hizo zingeingia kati ya juma la kwanza au pili la Machi.
Kasi ya ununuzi wa mashine hizo imekuwa ikusuasua kutokana na ukata wa fedha ambapo awali mahitaji yalikuwa mashine 15,000 lakini zilishushwa hadi 10,500 na baadaye 8,500.
Kati ya hizo 8,500, mashine 500 kwa mujibu wa Lubuva zitaenda kwa Shirika la Vitambulisho vya Taifa (Nida) kwa ajili ya uandikishaji Vitambulisho vya Taifa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment