Vitambulisho Vya Uzanzibari Vyazua Sokomoko

Vyama vya upinzani Zanzibar, vimeshauri Sheria ya Uzanzibari ya Ukaazi ifanyiwe marekebisho kabla ya utaratibu wa uandikishaji wapigakura unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.
Msimamo huo wameutoa baada ya Mkuu wa Divisheni ya Uchaguzi Zanzibar, Idrisa Haji Jecha kutangaza kuwa kazi ya uandishaji wapigakura wapya katika Daftari la Kudumu la Wapigakura litafanyika siku mbili kwa kila kituo baada ya kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa kufanyika Aprili 30.
Alisema Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeweka siku mbili za uandikishaji kwa kila kituo kutokana na muda mdogo uliobakia kuelekea uchaguzi mkuu kutokana na mambo mawili kufanyika kwa wakati mmoja.
Katibu Mkuu wa Chama cha Tadea, Juma Ali Khatib alisema kuwa sheria ya vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi kuna umuhimu wa kufanyiwa marekebisho kabla ya uandikishaji kuanza, kutokana na wananchi wengi kushindwa kumudu masharti ya kupata vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi.
“Wapo wananchi wengi hawana vyeti vya kuzaliwa na kumekuwapo na urasimu wa kupata fomu kutoka kwa viongozi wa serikali za mitaa (Masheha), lazima sheria irekebishwe kupunguza masharti ya kupata kitamburisho cha Uzanzibari Ukaazi,”alisema.
Khatib alisema pamoja na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010, imeshindwa kuondoa tatizo la upatikanaji wa vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi pamoja na vyeti vya kuzaliwa na kusababisha wananchi wengi kushindwa kupata haki ya kuandikishwa kuwa wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura visiwani humo.
“Pamoja na Rais, Dk Shein (Dk Ali Mohamed Shein) kuonyesha utendaji mzuri, wasaidizi wake wanamwangusha, wameshindwa kuondoa tatizo la upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa pamoja na urasimu wa fomu za kuwawezesha wananchi kupata Uzanzibari Ukaazi,” alisema Khatib.
 Alisema wakati umefika Baraza la Mawaziri kujadili sheria ya Uzanzibari Ukaazi na kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria kabla ya Baraza la Wawakilishi kuvunjwa baada ya kikao cha bajeti mwaka huu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omari Ali Shehe, alisema kuwa utafiti uliofanywa na chama hicho umebaini kuna watu karibu 12,000 hawajaandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kutokana na kukosa vyeti vya kuzaliwa na urasimu wa upatikanaji fomu za kuwawezesha kupata vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi kutoka kwa Masheha.
“Muda wa uandikishaji hautoshi na sheria inahitaji kuangaliwa upya kupunguza masharti ya sifa za kupata kitambulisho cha Uzanzibari Ukaazi, ili wananchi wengi waweze kupata haki ya kikatiba,” alisema Shehe.
Alisema kuwa kuna wazee wana miaka 60 hadi 70 wamekwama kupata vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi kutokana na kukosa vyeti vya kuzaliwa pamoja na kuwa wanaishi katika mtaa mmoja na Sheha, lakini bado wameshindwa kupewa fomu na kusajiliwa.


Shehe alisema ili uweze kukamilisha taratibu za kupata cheti cha kuzaliwa, karibu Sh35,000 zinahitajika kama gharama za ufuatiliaji, jambo ambalo limekuwa likiwashinda wananchi wengi kutokana na matatizo ya umaskini.
Credit: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment