Kwa Mujibu wa mtoto wa Marehemu Bw. Jerry Komba amesema kifo cha marehemu baba yake kimetokana na ugonjwa wa kisukari ambapo amedai kuwa sukari ilishuka ghafla akiwa nyumbani kwake Mbezi Beach Dar es salaam.
Taarifa za kifo hicho zimethibitishwa na Hospitali ya TMJ, ofisi ya Bunge na Chama Cha Mapinduzi na kwamba kwa sasa taratibu za maziko yake zinaendelea kufanywa .
Aidha taarifa za hivi punde kutoka nyumbani kwake maeneo ya Mbezi Beach Tangi Bovu zinaeleza kuwa maelfu ya watu kutoka katika kada mbalimbali wanaendelea kumiminika nyumbani kwa marehemu ili kutoa faraja kwa familia kwani marehemu ameacha mjane mmoja na watoto kumi na moja.
Akizungumza na tovuti hii mmoja wa madaktari aliyempokea wakati anafikishwa hospitali ya TMJ, Dk Elisha Ishan amesema Komba alifikishwa hospitalini hapo saa 10 jioni Jana akiwa mahututi .
"Nilimpokea nilianza moja kwa moja kumpima shinikizo la damu na vipimo vingine lakini tayari vilikuwa havifanyi kazi na hapo ndipo tukathibitisha kuwa ndugu yetu ameaga dunia," amesema Dk Ishan
Pamoja na hayo Dk Ishan amekwepa kutaja moja kwa moja chanzo cha kifo cha marehemu, hata hivyo amesema Kapteni Komba alikuwa na tatizo la shinikizo la damu na kwamba siku za karibuni alifika hospitalini hapo kwenye kiliniki yake ya shinikizo la damu.
0 comments:
Post a Comment