Kanisa la Pentekoste Tanzania Usharika wa Tandika, Manispaa ya Temeke limenusurika kuteketezwa kwa moto. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita na mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Chang’ombe.
Kaimu Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi (ACP), Zacharia Sebastian alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani leo baada ya taratibu kukamilika.
Akizungumza na gazeti hili katika ofisi yake, ambako ndiko moto huo ulianzia, Askofu wa Kanisa Jimbo la Temeke, Raymond Noya alisema tukio hilo ni la kushangaza, kwani halikulenga kuiba mali zilizokuwamo kwenye ofisi hiyo.
“Hili siyo suala la uhuni…naona inaweza kuwa ni vita dhidi ya imani. Lengo lilikuwa ni kuchoma kanisa na siyo kuiba vilivyomo. Kama unavyoona hakuna kilichoguswa wala jaribio la kuvunja ama mlango au dirisha. Hili ni jaribio la pili kutokea,” alisema Askofu Noya.
Kuhusu jaribio la kwanza alisema lilitokea Novemba mwaka jana, lakini hakukuwa na madhara makubwa na kesi ilifikishwa kituo cha polisi ingawa hadi leo haijafikishwa mahakamani kwa maelezo kuwa upelelezi bado unaendelea.
Noya alisema kwa miaka miwili iliyopita kumekuwa na matukio tofauti yanayokwaza huduma ya kanisa, kwani wakati mwingine wamekuwa wakirushiwa mawe wakati wa ibada.
“Kanisa lina mlinzi, lakini kuna wakati huwa anazidiwa. Tangu kanisa hili lilipoanzishwa mwaka 1997 ni miaka miwili tu iliyopita ndipo mambo yameanza kubadilika. Tumekuwa na ushirikiano mzuri na watu wanaotuzunguka kwa muda wote tuliokuwapo hapa,” alieleza.
Alphonce John, mkazi wa eneo lilipo kanisa alishangazwa na tukio hilo na kusema hakutegemea vitendo vya uharifu wa aina hiyo vinaweza kufanyika wakati huu.
“Wanapokuwa na sherehe watu wa mtaani huwa tunaalikwa na tunaenda kujumuika nao kwa chakula. Hakuna ugomvi wowote kati yetu. Hii inashangaza,” alisema John.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment