Kamati Kuu ya CCM imezidi kuwaweka gizani makada sita waliomaliza adhabu ya kufungiwa kwa miezi 12 baada ya kueleza kuwa uchunguzi dhidi yao unaendelea kwa muda usiojulikana, uamuzi utakaowazuia kujitokeza rasmi kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Edward Lowassa, Bernard Membe, Frederick Sumaye, William Ngeleja, Stephen Wasira na January Makamba, ambao walipewa adhabu hiyo Februari 18 mwaka jana, sasa watalazimika kusubiri hadi hapo Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM itakapomaliza uchunguzi wake, ikiwa imebaki miezi isiyopungua mitatu kabla ya wanachama kuanza harakati za kuwania nafasi mbalimbali.
Kwa kawaida, CCM huruhusu wanachama wake kuanza kuchukua fomu za kuwania urais, ubunge na udiwani kati ya mwezi Mei na Juni na kabla ya hapo huruhusiwa kutangaza nia ya kugombea nafasi wanazotaka, fursa ambayo makada hao wameikosa hadi sasa.
Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari jana baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu, kuwa kwa kuzingatia kanuni za maadili ya CCM, mwanachama aliyepewa onyo kali atakaa chini ya uangalizi kwa kipindi kisichopungua miezi 12,
“Baada ya miezi hiyo kwisha, Kamati Ndogo ya Maadili inaendelea na kazi yake kuchunguza mienendo yao hao waliokuwa wamepewa adhabu katika kipindi chao cha adhabu cha miezi 12 kama wametekelezaje masharti ya adhabu,” alisema Nnauye.
Alisema kazi ya kamati hiyo ndogo ni kuchunguza ili kubaini kama makada wote sita walitimiza masharti ya adhabu waliyopewa na kwamba itakapomaliza uchunguzi katika muda usiojulikana itapeleka taarifa Kamati Kuu.
“Itachukua wiki, itachukua mwezi, itachukua miezi ni kwamba itakapokamilika na Kamati Kuu kama kutakuwa na taarifa yoyote tutautaarifu umma juu ya kinachoendelea,” alisema Nnauye.
Kikao cha Kamati Kuu, ambacho huhusisha viongozi wa juu serikalini na kwenye chama hicho tawala pamoja na wanachama 14 wa kuchaguliwa kutoka Zanzibar na Bara, kilifanyika Ikulu na Nape aliongea na waandishi wa habari kwenye ofisi ya Umoja wa Vijana wa CCM iliyo Lumumba.
Kati ya waliofungiwa, Wasira, ambaye ni Waziri wa Kilimo na Ushirika, ni mjumbe wa Kamati Kuu.
Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, na Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ndiyo wanaochuana vikali na wafuasi wao wamekuwa wakishambuliana kwenye mitandao ya kijamii.
Sumaye pia alikuwa Waziri Mkuu kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu, wakati Ngeleja, ambaye amepewa adhabu kubwa zaidi kutokana na kuhusika kwake kwenye sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, alikuwa Waziri wa Nishati na Madini, na Makamba ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia.
Makada hao ambao walipewa kifungo cha miezi 12 Februari 18 mwaka jana, baada ya chama hicho kubaini kuwa walianza kupiga kampeni mapema kinyume na utaratibu wa CCM, bado hawajatangaza nia ya kutaka kuwania urais mwaka huu ingawa habari zinasema kuwa walishakusanya nguvu za kuanza mchakato huo baada ya kutoka kifungoni. Habari zinasema kuwa makada hao walikuwa wanasubiri uamuzi wa Kamati Kuu ili waingie rasmi kwenye kinyang’anyiro cha urais huku baadhi wakipanga hafla kubwa za kutangaza nia.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment