Mjadala kuhusu sakata la polisi kumpiga na kumtia mbaroni Profesa Ibrahim Lipumba jana ulikuwa mkali, lakini uliweka bayana kugongana kwa mihimili mitatu ya nchi baada ya Bunge kujadili suala hilo wakati likiwa limeshafika mahakamani.
Mgongano huo umetokea katika kipindi kisichozidi miezi miwili baada ya Bunge kugoma kupokea zuio la Mahakama la kujadili kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escow na kuendelea na mjadala ambao ulifikia maazimio ya kuwawajibisha wahusika.
Tukio lililojadiliwa jana lilitokana na Profesa Lipumba kukamatwa Jumanne wiki hii wakati akielekea Zakhem, Mbagala ambako alidai alikuwa akienda kutawanya wafuasi wa chama hicho baada ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano na mkutano wa hadhara wa chama hicho ulioandaliwa kwa ajili ya kukumbuka wafuasi 22 waliouawa mwaka 2001 wakati wakiandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.
Wakati mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia aliwasilisha hoja juzi majira ya saa 5.00 asubuhi kutaka Bunge lisitishe shughuli zake na kujadili suala hilo aliloliita “la dharura, kwa maslahi mapana ya Taifa”, Jeshi la Polisi lilimfikisha Profesa Lipumba mahakamani siku hiyohiyo lakini alasiri.
Jana, baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe kutoa taarifa ya Serikali kuhusu tukio hilo na kuomba radhi kwa yaliyotokea huku akiahidi uchunguzi kwa waliohusika kutumia nguvu kupita kiasi, Spika Anne Makinda alimsimamisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kuzungumza.
Masaju alijaribu kuzima mjadala huo kwa maelezo kuwa tayari Profesa Lipumba ameshafunguliwa mashtaka mahakamani, hivyo haingekuwa busara kwa Bunge kujadili suala hilo.
Kila alipojaribu kusoma vifungu vya sheria vinavyozuia muingiliano wa mihimili mitatu ya nchi, Serikali, Bunge na Mahakama, wabunge walipiga kelele.
Hata hivyo aliendelea kuwa Bunge linaongozwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria, na katika Kanuni ya 64 (1), Bunge haliruhusiwi kujadili jambo lolote ambalo liko mahakamani.
“Mihimili mitatu ni lazima isiingiliane, jambo hili lipo bungeni kujadiliwa kwa ajili ya kutolewa maamuzi, na lipo mahakamani kwa ajili ya kutolewa maamuzi, lakini mahakama ndiyo inayoweza kutoa maamuzi ya mwisho,” alisema Masaju.
“Kutokana na mazingira haya, naomba nilishauri Bunge lisijadili jambo hili,” alisema mwanasheria huyo aliyeteuliwa mapema mwezi huu.
Lakini baada ya kumaliza hoja zake, wabunge walipiga kelele na baadhi wakisema wanataka muongozo. Baadaye Spika Makinda alisema Bunge litajadili suala hilo.
Wabunge walijadili kwa kina tukio lote la kupigwa na kukamatwa kwa Profesa Lipumba kujaribu kuonyesha kuwa kiongozi huyo hakufanya kosa kwa kuwa chama kilifuata taratibu zote za kulitaarifu Jeshi la Polisi na kwamba baada ya amri ya kuzuia maandamano na mkutano, alitii amri, hoja ambazo zinaonekana kupinga mashtaka yaliyoko mahakamani kuwa Lipumba na wafuasi 32 wa CUF waliandamana bila ya kibali.
0 comments:
Post a Comment