Shahidi wa pili katika kesi inayomkabili kiongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (pichani), wamekana mbele ya Mahakama ya Hakimu mkazi wa mkoa wa Morogoro, kuwa hawakuhusika kumpiga risasi kiongozi huyo na kwamba Sheikh Ponda alikamatwa jijini Dar es Salaam akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akitibiwa jeraha lililodaiwa kuwa ni la kupigwa risasi.
Akitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo, shahidi huyo ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ( RCO) wa mkoa wa Morogoro, Japhet Kibona, alidai kuwa Agosti 9 , 2013, Polisi walipata taarifa za kiinterejensia kuwa Sheikh Ponda angefika mkoani Morogoro kwa ajili ya kuhudhuria kongamano la Eid pili, hivyo polisi iliwataka waandaji wa kongamano hilo kumsalimisha polisi kiongozi huyo.
Kibona ambaye kwa sasa ni RCO wa mkoa wa Mtwara, alidai kuwa polisi walitaka Sheikh Ponda ajisalimishe kwa sababu alikuwa akitafutwa kutokana na tuhuma za kutoa maneno ya kashfa na uchochezi jijini Dar es Salaam na Zanzibar.
Alidai kuwa Sheikh Ponda alikaidi amri hiyo ya kujisalimisha, badala yake alifika mkoani Morogoro na kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Waislamu na serikali huku akihusisha gesi iliyogunduliwa Mtwara na mgogoro wa ardhi wa Loliondo pamoja na kamati za ulinzi na usalama za kwenye misikiti na kuwataka Waislamu kufunga milango na madirisha kisha kuwapiga watu wataojitambulisha kuwa ni kamati hizo kwenye misikiti.
Alisema baada ya Sheikh Ponda kutoa maneno hayo ambayo yaliumiza imani za dini na kukiuka masharti ya kibali kilichotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro (OCD) na yeye kama RCO aliwapanga askari kwa ajili ya kumkamata Ponda, lakini askari hao walishindwa kutokana na wingi wa watu waliohudhuria kongamano hilo.
Alieleza kuwa katika harakati za kumkamata ghafla Sheikh Ponda bahati mbaya aliigizwa ndani ya gari dogo na wafuasi wake na kumpeleka kusikojulikana.
Kibona alidai kuwa baadaye alipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuwa Sheikh Ponda alijeruhiwa kwa risasi katika bega la mkono wa kulia.
Aliongeza kuwa akiwa na maofisa wenzake walikwenda katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro, lakini Sheikh Ponda hakuwapo na siku iliyofuata alipata taarifa kuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbiri.
Wakili wa Sheikh Ponda, Juma Nassoro, alimuuliza shahidi huyo kuwa nani alimpiga risasi Sheikh Ponda ikiwa polisi ndiyo walikuwa na silaha za moto katika kongamano hilo na je anafahamu kuwa mmoja kati ya askari waliokuwapo kwenye kongamano hilo alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda na je, kikosi hicho kilishindwa nini kumkamata Sheikh Ponda ambaye hakuwa na silaha yoyote?
Kibona akijibu maswali hayo huku akiongozwa na wakili mkuu mwandamizi wa Serikali, Benard Kongola, alidai kuwa hafahamu kama kuna askari aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda na kwamba hawezi kufahamu nani aliyehusika kumpiga risasi.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 2 mwaka huu.
Chanzo: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment