CHADEMA, CUF Wahoji Usafi wa Rais Kikwete Wamtaka Atangaze Mali Zake, Wadai Naye ni Fisadi

KAULI mbiu ya ‘kujivua gamba’ ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaendelea kuwa mwiba mchungu kwa chama hicho baada ya wananchi kuhoji nguvu ya kimaadili ya Rais Jakaya Kikwete ambaye anadai kutaka kuondoa mafisadi ndani ya chama huku naye akihusishwa na ufisadi mwingine.

Baadhi ya viongozi na makada wa CCM na vyama vya upinzani wamedai jitihada za Rais Kikwete kushambulia na kuadhiri wanasiasa wenzake kwa kumtumia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, ni za kinafiki, kwani naye (Kikwete) yu miongoni mwa mafisadi.

Jana ilikuwa zamu ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, na Diwani mstaafu wa Tarime (CHADEMA) John Heche, ambao kwa nyakati tofauti walisema CCM haisafishiki.
Walisema ili kuisafisha CCM na serikali yake, ingepaswa kuwaondoa wote waliotajwa kwenye ufisadi akiwemo Rais Kikwete.

Profesa Lipumba aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya CUF.

Mbali na ufisadi wa Kikwete uliotajwa na Dk. Willibrod Slaa Septemba 2007, jana Profesa Lipumba aliongeza mali za Kikwete.

Alisema Rais Kikwete aligoma kutangaza mali zake alipoingia madarakani na hata sasa hataki kufanya hivyo kwa sababu kuna harufu ya ufisadi katika mali hizo.

Profesa Lipumba alidai kuwa Rais Kikwete, kama angekuwa mtu safi angetangaza mali zake kabla hajaingia Ikulu kama alivyofanya mtangulizi wake, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ili wananchi wapime uadilifu wake.

“Kama kweli Rais Kikwete ana nia ya kupambana na ufisadi atangaze mali zake na wale wote wanaotuhumiwa wafunguliwe mashtaka na wafikishwe mahakamani.

“Najua katika hili, Rais Kikwete hawezi, kwani anahofia wale waliopewa siku 90 watatoa siri kubwa pamoja na kuwataja vigogo walionufaika na ufisadi wao. Hiki ni kipimo kuwa CCM haina uwezo wa kupambana na ufisadi ila inachofanya ni usanii dhidi ya ufisadi,” alisema Profesa Lipumba.

Hata hivyo alisema kamwe CCM haiwezi kuwachukulia hatua watuhumiwa hao wa ufisadi kwa kile alichodai kuwa tuhuma hizo zinawagusa vigogo wengi wa CCM ambao kama walivyoshindwa kuchukua hatua dhidi ya kampuni ya Kagoda na mafisadi wa EPA, haiwezi kuwagusa hata hawa.

Kuhusu ununuzi wa rada, alisema kama kweli serikali ina nia ya kupambana na ufisadi, itumie ushahidi ulioletwa na Ofisi ya Upelelezi wa Makosa Makubwa ya Uingereza (SFO) kuwafikisha mahakamani vigogo wote waliohusika na sakata la ununuzi wa rada kwani hadi sasa hakuna ofisa yeyote aliyekamatwa.

Kuhusu mchakato wa kubinafsishwa kwa mashirika ya umma hasa kampuni ya sigara na kampuni ya simu, Lipumba alisema makampuni hayo yaliuzwa kwa bei ndogo kuliko thamani yake.
Kutoka Mwanza, Heche aliweka wazi kwamba kauli zinazotolewa na Nape ni tambo na hadaa kwa wananchi kwa vile amekubali kuwa vuvuzela la mafisadi.

Heche alisema hayo katika mkutano wake na vyombo vya habari, huku akitangaza nia yake ya kuwania uenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA).

Alisema Nape anatoa kauli za kitoto za kudai kuwa Dk. Willbrod Slaa anatumiwa na mafisadi ili amshambulie Rais Kikwete na familia yake, kwa kuwa Dk. Slaa ndiye aliyewataja hao mafisadi, Kikwete akiwamo; na kwamba vita ya ufisadi ni ya CHADEMA si ya CCM.

“Nape anadiriki kusema hayo kwa sababu badala ya kueneza itikadi za CCM anajigeuza vuvuzela la mafisadi. Ameamua kuwa mweneza propaganda badala ya itikadi. Hatuwezi kumsikiliza hata kidogo.

“Ingawa kwa juujuu anajifanya kupambana na ufisadi, Nape hana uwezo wala uadilifu wa kukemea mafisadi kwa sababu hata Rais Kikwete anayemtetea ametajwa kwenye orodha ya mafisadi kule Mwembeyanga.

“…Ningependa kumuuliza Nape katika orodha ya mafisadi 16 waliotajwa na Dk. Slaa, yeye anamtetea fisadi yupi? Anajua kwamba hata Rais Kikwete alitajwa? Ni lini Nape amepewa ajira ya kutetea udhaifu binafsi wa Rais na familia yake?” alihoji Heche kupitia taarifa hiyo.

“Tumeushtukia mpango wa CCM kuidhoofisha hoja ya CHADEMA inayolenga kupambana na mafisadi wanaotafuna fedha za Watanzania na hatuko tayari kuukubali,” alieleza Heche.

Alisema wote wanaotaka kuondoa ufisadi nchini lazima wautazame kwa marefu na mapana, wajue na wakubali kusema wazi kwamba Rais Kikwete mwenyewe ni zao la ufisadi. Pesa za EPA zilizoibwa Benki Kuu zilitumika kununua urais wake.

“Tunaamini kwamba Watanzania walishagundua ukweli huu, ndiyo maana mwaka 2010 hawakumpa Rais Kikwete kura za kutosha kama mwaka 2005 wakati anaingia. Hivyo, wote wanaomtetea akiwemo Nape, wanatetea ufisadi. Wanahujumu Watanzania.

“Enzi za CCM kuendelea kuongoza Watanzania zimekwisha. Hii ni zamu ya Watanzania wanaotafuta matumaini mapya kupitia CHADEMA,” alisisitiza Heche.

Akizungumzia azima yake ya kusaka uongozi wa BAVICHA, Heche alisema: “Kwa kuwa mimi ni mwanachama makini wa CHADEMA na kwa kuwa nimewahi kuwa kiongozi sasa nawania uongozi tena, naona ni vema nitumie fursa hii kuzungumzia masuala kadhaa ninayoshuhudia yakisemwa au yakifanywa na chama tawala kinachokaribia kumaliza muda wake.” 

Aidha, aliwaomba vijana wote kuwa makini zaidi katika kuitengeneza Tanzania mpya kwa mustakabali wa vizazi vijavyo na kubainisha kwamba kazi ya BAVICHA ijayo chini ya uongozi wowote utakaochaguliwa ni kuwainua vijana katika kuwamulika mafisadi wote hata kama wapo madarakani.

CHADEMA kinatarajiwa kufanya uchaguzi wa BAVICHA uliofutwa miaka miwili iliyopita baada ya uongozi wa chama kuridhika kwamba taratibu za uchaguzi zilikosewa.

Heche anakuwa mwanachama wa kwanza kutangaza nia hiyo. Alitaja sababu tisa za kugombea uongozi BAVICHA. Alisema:

“Kwanza mimi ni mwana CHADEMA kijana. Nafasi inayogombewa ni ya vijana. Hii ni fursa kwangu kuitumia vema haki yangu ya kugombea uongozi wa vijana ndani ya chama.

“Dhamira yangu ni kuifanya BAVICHA kuwa taasisi imara, ambayo itakuwa tanuru la viongozi makini katika ngazi mbalimbali, kichama na kitaifa. BAVICHA ni chombo kipya. Uchaguzi huu ni sehemu ya mchakato wa kukianzisha, kukijenga na kukiimarisha, ili kiwe kimbilio la vijana wengi wa taifa hili wanaotaka mabadiliko.

“Katika kuisuka BAVICHA kutoka ngazi ya kata hadi taifa, tutakuwa tumeunganisha nguvu za vijana wa Tanzania katika kudai uhuru wa kweli, usawa na haki.

“Nataka kuendeleza jitihada za viongozi na makada wetu za kupigania ushiriki wa vijana katika siasa za Tanzania na uongozi.

“Nataka kuijenga BAVICHA iwe daraja la kuwafikia, kuwainua na kuwajenga vijana wasomi walio vyuoni na waliohitimu waweze kushiriki siasa za ukombozi wa taifa lao.

“Ningependa, kupitia BAVICHA, kusimika mapambano ya ukombozi ya aina yake Tanzania Visiwani, kwa kuanzisha kanda maalumu ya BAVICHA visiwani, kama moja ya mikakati ya chama ya kukikuza CHADEMA miongoni mwa vijana na jamii ya Zanzibar.

“Nataka kuifanya BAVICHA kuwa chachu ya mafunzo kwa vijana juu ya falsafa na itikadi za chama katika ngazi za majimbo, wilaya na mikoa.

“Nataka kuongoza taasisi itakayosaidiana na taasisi nyingine rasmi na zisizo rasmi katika kusimamia, kuwajibisha na kuihoji serikali kuhusu masuala muhimu yanayohusu maisha ya Watanzania.

“Nataka kuongoza vijana, kupitia BAVICHA, kuendelea kudai serikali ianzishe Baraza la Vijana la Taifa.” 



Source: Tanzania Daima
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment