Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanza mjini Dodoma, sasa hakuna shaka kwamba Rais Jakaya Kikwete atafanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri wakati wowote kuanzia leo na kabla ya Jumapili (saa 48) kutokana na kukabiliwa na safari ya nje.
Rais anatarajiwa kufanya mabadiliko hayo baada ya kumwondoa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow baada ya kuingiziwa Sh1.6 bilioni kwenye akaunti yake.
Mwingine ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye anatuhumiwa kutoshughulikia kwa makini sakata hilo na kusababisha Serikali kupoteza fedha hivyo kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa kumvua uwaziri utakaomlazimu Rais kufanya mabadiliko madogo kwenye baraza lake, ikiwa ni miezi isiyozidi mitano kabla ya kuvunja Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa Rais Kikwete anaweza kutangaza mabadiliko hayo wakati wowote kuanzia leo.
“Rais anaondoka Jumapili kwenda Davos (Uswisi kuhudhuria mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia (WEF)), hivyo kwa jinsi yoyote ile ni lazima atangaze baraza kesho (leo) au Jumamosi,” alisema mpashaji habari wetu.
“Hawezi kutangaza baraza jipya akiwa nje ya nchi, hivyo ni lazima atangaze kesho (leo) au ikishindikana Jumamosi ili Jumapili afanye shughuli nyingine na kuondoka.”
Hata hivyo, mabadiliko ya mwisho ya Baraza la Mawaziri yalitangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ambaye pia anaweza kupewa kazi hiyo.
Baada ya kujadili sakata la uchotwaji wa fedha hizo kwa takriban siku nne, Novemba 28, mwaka jana Bunge lilifikia maazimio manane, likiwamo la kutaka wote waliohusika kwenye kashfa hiyo wachukuliwe hatua na mamlaka husika, akiwamo Profesa Muhongo ambaye Rais Kikwete alisema Novemba 22, 2014 kuwa amemuweka kiporo hadi baada ya “siku mbili au tatu” kusubiri matokeo ya uchunguzi.
Hata hivyo, shinikizo liliongezeka baada ya Kamati Kuu ya CCM, iliyokutana Zanzibar chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, kuitaka Serikali iwe imetekeleza kwa vitendo maazimio yote ya Bunge kuhusu sakata hilo kabla ya kikao cha Bunge kitakachoanza Jumanne ijayo na kutaka wahusika walioko kwenye dhamana za uteuzi wachukuliwe hatua stahili na mamlaka zao kuwawajibisha mara moja.
Pia, Kamati ya Maadili ya CCM iliyokutana Dar es Salaam mapema wiki hii, iliwajadili wanachama waliohusika kwenye kashfa hiyo na kupeleka taarifa yake kwenye Kamati Kuu ya chama hicho kwa hatua zaidi.
Wakati CCM ikisema hayo, wabunge wamekuwa wakimkumbusha kiongozi huyo wa Serikali kuchukua hatua kabla ya kikao cha Bunge. Wabunge wawili wa mkoani Arusha, Godbless Lema na Joshua Nassari wote kupitia Chadema, wamediriki kusema kuwa watamwondoa Profesa Muhongo kwa mabavu kwenye ukumbi wa chombo hicho cha kutunga sheria iwapo Rais hatakuwa amemuondoa.
Pia, nchi wahisani zilieleza mapema mwezi huu kuwa pamoja na kuruhusu kiasi cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, bado zinasubiri tamko la Serikali kuhusu sakata hilo, ikiwa ni pamoja na hatua ilizochukua kuzuia kashfa kama hiyo isitokee tena, ili Tanzania inufaike kwa misaada hiyo ya fedha zinazotokana na walipakodi wa nchi zao.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment