PAC Yaibua Ufisadi Mwingine

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeanika madudu na kashfa za kutisha katika ripoti maalumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikiwa ni pamoja na zaidi ya Sh100 bilioni kukwepwa kulipwa na kampuni mbalimbali kwa kivuli cha misamaha ya kodi.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa jana na Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe imeeleza ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, jinsi ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA), ulivyofanyika bila kibali kutoka Baraza la Mawaziri, huku mchango wa ujenzi wa jengo hilo kwa Serikali ukiongezwa kwa Sh2.3 bilioni.
Pia, imeibua udanganyifu uliofanyika katika nyumba za Bodi ya Korosho na Bodi ya Sukari ambazo kwa sasa zinatumiwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvestry Koka.
Alisema hadi kufikia Juni 30, 2013 misamaha ya kodi iliyokuwa imetolewa ilikuwa Sh 1.5 trilioni lakini hadi Juni 2014, misamaha hiyo iliongezeka kwa asilimia 22.6 mpaka kufikia Sh 1.8 trilioni.
Zitto alisema: “Mwaka 2012/13, CAG alibaini ukiukwaji wa maelekezo ya Serikali uliosababisha hasara ya Sh22.3 bilioni kutokana na kuhamishwa kwa mafuta yenye msamaha wa kodi kutoka kwa kampuni za madini kwenda kwa makandarasi mbalimbali.”
Alisema Kampuni ya M/S Geita Gold Mines na Resolute Tanzania Limited zilihamisha mafuta yaliyosamehewa kodi yenye thamani ya Sh22.3 bilioni kwenda kwa makandarasi mbalimbali (M/S Geita Gold Mines, Sh22 bilioni na Resolute Tanzania Limited, Sh20 milioni).
Alisema uhamishaji huo ulikuwa ni kinyume na tangazo la Serikali la Oktoba 25, 2002 lililoelekeza kusitisha msamaha wa kodi pale ambako mafuta yaliyosamehewa kodi yatatumika kwa matumizi tofauti na yaliyokusudiwa au yatahamishiwa, kuuzwa au kupewa mtu mwingine ambaye hana haki ya kupewa msamaha huo.
Alisema matumizi ya misamaha ya kodi kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa pia yalisababisha upotevu wa mapato ya Sh392.7 milioni.
“Mwaka 2011/2012 na 2012/2013 Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd ya Arusha iliagiza magari 28 na kusamehewa kodi yenye thamani ya Sh465 milioni, lakini ukaguzi maalumu umebaini kuwa kampuni hiyo inamiliki magari mawili tu ambayo si kati ya yale 28 yaliyoingizwa nchini kwa msamaha wa kodi,” alisema na kuongeza: “Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato (Arusha) ilikiri kuwa baadhi ya magari hayo yalisajiliwa na TRA na yanatumiwa na watu binafsi ambao hawakuwa na haki ya kupewa msamaha wa kodi.”
Alisema ripoti hiyo pia inaeleza jinsi misamaha ya kodi iliyotolewa kwa kampuni isiyostahili yenye thamani ya Sh53.3 milioni.
“Kampuni ya Kilemakyaro Mountain Lodge Limited ilipewa msamaha wa kodi kwa ajili ya mradi wa ujenzi na upanuzi wa hoteli kadhaa katika Kijiji cha Changarawe wilayani Karatu, Arusha. Ukaguzi Maalumu umebaini kuwa Kampuni hiyo iliagiza magari matatu kwa kutumia msamaha huo wa kodi na magari hayo yalipata msamaha wenye thamani ya Sh72.6 milioni.”
Inaeleza kuwa wakaguzi walipokwenda kukagua mradi huo, hawakukuta gari hata moja ingawa menejimenti ya kampuni ilithibitisha ununuzi wa gari moja tu na haikuwa na taarifa ya ununuzi wa hayo mengine.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment