Serikali Imekubali Kuchukua Madeni Yote ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) na Kuyalipa

SERIKALI imekubali kuchukua madeni yote ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) na kuyalipa, baada ya uhakiki ili kutoa fursa kwa shirika hilo kuanza biashara.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Monica Mwamunyange, alisema hayo jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kuongeza kuwa kinachofuatia ni kuunda upya shirika hilo.

“Shirika hilo litaundwa upya, ikiwa ni pamoja na kumtafuta kiongozi wake kwani Mkurugenzi wa sasa atastaafu mwezi ujao, ikiwa ni pamoja na kupunguza wafanyakazi na kubaki na nguvu kazi yenye tija, kwani kwa sasa tuna ndege moja lakini kuna wafanyakazi 140,” alisema.

Ndege mpya Mbali na kuundwa upya kwa kampuni hiyo, Mwamunyange alisema Serikali inaendelea na mchakato wa kununua ndege mbili aina ya D8-Q400 kutoka kampuni ya Bombardier Canada, kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 32.87 kwa kila moja.

Ndege hizo kwa mujibu wa Mwamunyange, zitanunuliwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB) na zitatumika kutoa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani na kikanda.

Mbali na ndege hizo mpya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Kapteni Milton Lazaro alisema kwa sasa Kampuni hiyo inamiliki ndege moja aina ya Dash 8-Q300 ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 50.

Kwa mujibu wa Kapteni Lazaro, kwa sasa ndege hiyo ipo kwenye matengenezo kuanzia Oktoba 24, mwaka jana na inatarajiwa kukamilika Februari 2015, ila kwa sasa kampuni hiyo imekodisha ndege mbadala moja.

Madeni Akifafanua uchukuaji wa madeni hayo, Mwamunyange alisema Serikali inafanya majadiliano na baadhi ya wadai wa kampuni hiyo, kuangalia uwezekano wa kuondoa riba ili kupunguza deni la msingi na gharama nyinginezo.

“Majadiliano na kampuni nne yamekamilika na wamekubali kuondoa gharama zinazofikia bilioni 17.13 katika deni lao,” alisema. Mwamunyange pia alisema kampuni hiyo inakamilisha mpango wa biashara wa kampuni, utakaoonesha mahitaji ya ATCL kwa miaka mitano hadi kumi, utakaoainisha mahitaji ya rasilimali watu na kuwasilishwa serikalini.
Alisema mpango huo wa kibiashara ambao uko katika hatua za mwisho, pia utaonesha mwelekeo huku wakitarajia kushirikisha sekta binafsi.

Wawekezaji Alisema pia Serikali itaendelea kutafuta wawekezaji kwani awali baadhi ya kampuni za wawekezaji hazikuwa na sifa, na baadhi zilikuwa na masharti ambayo hayana manufaa kwa ATCL, huku zingine zikisita kuwekeza kutokana na deni kubwa la shirika hilo.
Alisema changamoto zingine zinazoikabili ATCL ni ukosefu wa vitendea kazi na wataalamu wa ndege ambao ni marubani na wahandisi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment