Wafuasi 30 wa Chama cha Wananchi CUF wanaokabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama na kukaidi amri halali ya polisi na kufanya maandamano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana waliyopewa.
Hakimu Mkazi, Emillius Mchauru jana aliwaachia huru washtakiwa hao baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika na kila mdhamini asaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh 100,000.
Baada ya washtakwia hao kukamilisha masharti hayo ya dhamana, Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi Februari 12,2015 kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Juzi, Mawakili wa Serikali, Joseph Maugo na Hellen Mushi, katika shtaka la kwanza alidai kuwa Januari 27,2015 katika eneo la Temeke washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kufanya uhalifu.
Akisoma hati hiyo ya mashtaka, Maugo katika shtaka la pili alidai kuwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa 28 kati ya 30 wanaokabiliwa na kesi hiyo, wakiwa katika ofisi ya CUF karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke bila ya kuwa na uhalali walifanya mkusanyiko kwa nia ya kufanya maandamano kuelekea Mbagala Zakhem.
Katika shtaka la tatu, ambalo nalo pia linawakabili washtakiwa 28 kati ya 30 , Wakili huyo wa Serikali, Maugo alidai kuwa siku hiyo hiyo ya tukio katika eneo la Mtoni Mtongani waligoma na kutojali tangazo halali lililotolewa na polisi lisilowaruhusu kuandamana na hata kufanya mkusanyiko usio halali.
Washtakiwa wanaokabiliwa katika kesi hii ni Shabani Ngurangwa (56), Shabani Tano(29), Shabani Abdallah (40), Juma Mattar (54), Muhamed Kirungi (40), Athuman Ngumwai (40), Shaweji Mohamed(39), Abdul Juma(40), Hassan Said (37), Hemed Joho (46) na Mohamed Ibrahim (31).
Pamoja na Issa Hassan (53), Allan Ally(53), Kaisi Kaisi (51), Abdina Abdina (47), Allawi Msenga (47), Mohamed Mtutuma (33), Salehe Ally (43), Abd Hatibu (34), Bakari Malija (43), Abdallah Ally(32) , Said Mohamed (40), Salim Mwafisi, Salehe Rashid (25), Abdallah Said(45),Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42), Athuman Said (39).
Kwa upande wa washtakiwa Dickson Leasson (37) na Nurdin Msati (37) wao hawahusiki katika shtaka la pili na tatu ambayo yanawakabili wenzake.
0 comments:
Post a Comment