Yanga imemburuza mahakamani mlinda mlango wao, Juma Kaseja wakitaka awalipe Sh340 milioni ikiwani fidia.
Yanga wamefikia uamuzi huo Ijumaa iliyopita baada ya kufikisha kesi Mahakama ya Kazi na tayari Kaseja ameshapewa notisi ya kuitwa mahakamani kujibu shtaka la kukacha timu yake ikiwa ni pamoja na kulipa kiasi hicho cha fedha.
Yanga wanataka Kaseja awalipe Sh340 milioni ikiwa ni ada ya usajili, ambayo ni Sh40 milioni pamoja na fidia ya Sh300 milioni ambazo ni gharama za usumbufu wa kuvunja mkataba, kumhudumia na kutunza kiwango chake kwa kipindi chote alichokuwa Yanga.
Mmoja wa viongozi wa Yanga aliliambia gazeti hili kuwa kuna nyaraka ambazo Yanga wanatakiwa kuzikamilisha ili wapangiwe hakimu wa kusikiliza kesi hiyo ambayo itafungua ukurusa mpya wa bifu na kisasi miongoni mwa Yanga na mlinda mlango huyo.
Wakili wa Yanga, Frank Chacha alikiri klabu hiyo tayari imeshamfungulia mashtaka Kaseja na kesho wanategemea kupangiwa hakimu wa kusikiliza shauri hilo.
Kaseja aliingia kwenye mgogoro na uongozi wa Yanga baada ya Novemba 11 mwaka jana kuandika barua ya kuvunja mkataba na klabu hiyo baada ya kukiuka makubaliano ya mkataba kati yao akishinikiza kulipwa Sh20 milioni za usajili alizokuwa anaidai klabu hiyo.
Kaseja kupitia Kampuni ya Mbamba Advocate iliandika barua ya kuvunja mkataba na klabu hiyo kwa kile ilichoeleza kuwa amekuwa akisugua benchi. Pia, uongozi wa Yanga umekiuka makubaliano baina ya pande mbili ambazo hadi Januari mwaka huu walitakiwa kummalizia ada yake ya usajili Sh20 milioni, lakini hata hivyo haikufanya hadi alipowasilisha barua ya kuvunja mkataba.
Akizungumza na gazeti hili, Wakili wa Kaseja, Samson Mbamba alikiri kupokea notisi hiyo ya mashtaka dhidi ya mteja wake.
Meneja wa Kaseja, Abdulfatah Saleh, hakuweza kupatikana jana ili kueleza msimamo wa mchezaji huyo ambaye yuko nje ya timu tangu mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment