RAIS Jakaya Kikwete sasa ametengwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika matamanio yake ya kutaka Katiba mpya ya Tanzania ipatikane kabla ya kumalizika kwa mwaka 2015.
Pamoja na Ukawa, kundi jingine lililoonyesha kujitenga naye katika matamanio yake hayo ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambacho kimeitaka Tume ya Uchaguzi kuahirisha zoezi la upigaji kura ya maoni hadi pale daftari la wapiga kura litakapokamilika.
Viongozi wa Ukawa jana waliitisha mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) na kutangaza kuwa wanachama na mashabiki wake hawatashiriki upigaji wa kura ya maoni ya kupitisha Katiba Mpya unaotarajiwa kufanyika Aprili 30.
Katika tangazo lao hilo, walisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa mchakato uliotumika kufikia upigaji wa kura ya maoni ni batili.
Akitoa tangazo hilo kwa niaba ya viongozi wenzake wa Ukawa, Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wana Ukawa wataungana na wananchi wote wanaopinga mchakato huo kuhakikisha Katiba Mpya haipiti.
Alisema katika mkutano wa viongozi wa Ukawa uliofanyika wiki hii Dar es Salaam, waliafikiana kuendelea na msimamo wa kususia mchakato mzima wa uandikaji wa Katiba mpya kwa sababu haufuati matakwa ya wananchi.
“Ukawa hatutashiriki kura ya maoni ya Katiba Mpya na tunawaomba Watanzania waungane nasi katika msimamo huu wa kupinga mchakato batili unaofanywa na CCM,” alisema Profesa Lipumba.
Aidha, Prof. Lipumba alisema mwenendo wa uandikishaji wa daftari la wapigakura hauridhishi kwa sababu wananchi wa Zanzibar wanakabiliwa na hatari ya kufanyiwa uamuzi na wenzao wa Tanzania Bara wakati wa upigaji kura ya maoni.
Alisema visiwa vya Zanzibar na mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro kupangwa mwisho katika uandikishaji huo kutawachanganya wananchi wengi na huo unaweza kuwa mkakati wa CCM wa kupenyeza wananchi wa Tanzania Bara kupiga kura ya maoni upande wa Zanzibar.
Maelezo hayo Prof. Lipumba yaliungwa mkono Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Dk. Emanuel Makaidi, ambaye alisema mchakato wa upigaji kura ya maoni umeanza kufanyiwa kazi na CCM.
Alisema tayari baadhi ya wananchi wa Tanzania Bara wameanza kupelekwa Zanzibar kwa ajili ya kujiandikisha.
Makaidi alimshambulia kwa maneno makali Rais Jakaya Kikwete kwa kueleza kuwa ana tabia ya ukigeugeu kwenye uamuzi wa msingi na kwenda mbali kwa kumfananisha na kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hayati Mobutu Sese Seko.
“Sijawahi kuona rais kigeugeu kama huyu na hata nikimlinganisha na Mobutu Sese Seko naona yeye ni zaidi yake. Tumekutana kwenye jukwaa la vyama vya siasa na tukakubaliana asitishe mchakato, lakini tulipoachana mwenzetu akatugeuka.
“Sasa tunawaomba wananchi watuunge mkono katika msimamo huu wa kutokuipigia kura Katiba Mpya,” alisema Dk. Makaidi.
“Sasa tunawaomba wananchi watuunge mkono katika msimamo huu wa kutokuipigia kura Katiba Mpya,” alisema Dk. Makaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, alisema Ukawa umechukua uamuzi wa kujitenga ili kupisha kile alichokiita zoezi haramu linaloendeshwa kwa ajili ya kupata Katiba haramu ambayo haijaridhiwa na wananchi.
Mbowe aliwataka Watanzania kuunga mkono juhudi za Ukawa za kususia upigaji kura ya maoni na kuonya kuwa endapo Katiba mpya itapitishwa na wananchi, nchi inaweza kuingia kwenye machafuko.
Aliilaumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwaandikisha wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura bila kuwaelimisha.
0 comments:
Post a Comment