JK Azuia Mawaziri Kutoka Nje ya Dar

Mawaziri wote wamezuiwa kusafiri kikazi nje ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na kile kinachoelezwa ni maandalizi ya kukabidhi ofisi kwa mawaziri wapya ambao wanatarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa.
Taarifa hizo zimekuja siku moja tu tangu Ikulu kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salvatory Rweyemamu, kuwataka Watanzania kuwa na subira kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati wowote kuanzia sasa atatoa uamuzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Profesa Muhongo na baadhi ya viongozi wengine wa Serikali, wanahusishwa na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Jana, vyanzo mbalimbali vya habari serikalini, vililidokeza MTANZANIA kuwa mawaziri wote sasa wamezuiwa kusafiri nje ya Dar es Salaam kutokana na kusubiri mchakato huo wa kukabidhi ofisi.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, karibu mawaziri wote na naibu mawaziri walikuwapo jijini Dar es Salaam jana isipokuwa wachache ambao haikuthibitika mara moja kama walikuwapo au la.
Vyanzo hivyo viliongeza kwamba tayari Rais Kikwete amekwishamaliza mchakato wa uteuzi na baraza jipya la mawaziri, ikiwa yupo nchini Uswisi katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia.
“Ni kweli tumepokea maagizo ya kutosafiri nje ya Dar es Salaam, lakini kwa hili ni hofu tupu, si suala la mabadiliko madogo ya kawaida kama Bunge lilivyoazimia.
“Nina hofu huenda Rais Kikwete anataka kufanya mabadiliko makubwa kwa baraza lote la mawaziri, acha tusikilize hadi mwisho nini kitaendelea maana ni presha tupu sasa,” kilisema chanzo chetu.
Kwa miezi miwili sasa nchi imegubikwa na mjadala kwa watu wa kada tofauti kushinikiza kufanyika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri baada ya Bunge kupitisha maazimio manane likiwamo la kutaka kufutwa uteuzi wa mawaziri waliotajwa kuhusika na sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mawaziri wanaotakiwa kuwajibishwa kwa kufutwa uteuzi wao kutokana na maazimio hayo, ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo pamoja na Profesa Anna Tibaijuka ambaye tayari Rais Kikwete alitangaza kufuta uteuzi wake wa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Desemba 22, mwaka jana.
Viongozi wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ambaye amesimamishwa kupisha uchunguzi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye amejiuzulu.
Juzi katika mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rweyemamu, alisema taratibu za kumwajibisha Profesa Muhongo kama kiongozi wa kisiasa hazifanani na hatua zilizochukuliwa kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Maswi kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Serikali.
Akizungumzia ziara za Profesa Muhongo anazoendelea nazo mikoani, Rweyemamu alisema tuhuma hizo hazimzuii kufanya kazi kwa kuwa bado hajaondolewa kwenye nafasi ya uwaziri aliyonayo.
Desemba 22, mwaka jana, Rais Kikwete akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema amemuweka kiporo Profesa Muhongo maana bado hajapata ufafanuzi kuhusu mambo kadha wa kadha, na kwamba baada ya siku mbili, tatu hivi atakapopata ufafanuzi na kujiridhisha, atachukua uamuzi.
Siku nne baadaye, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema Rais Kikwete bado hajakamilisha kulishughulikia suala hilo na kwamba litakapokuwa tayari wananchi watajulishwa hatua alizochukua.
Ikiwa Rais Kikwete atafanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, itakuwa ni mara ya nne kufanya hivyo tangu aingie madarakani mwaka 2005.
Kwa mara ya kwanza alifanya mabadiliko mwaka 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa kujiuzulu kutokana na sakata la Richmond.
Mei 4, mwaka 2012 Rais Kikwete alifanya tena mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri baada ya Bunge kutaka mawaziri wanane waliotajwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh wawajibike au wawajibishwe.
Mawaziri waliotakiwa kuwajibishwa baada ya kushindwa kuwajibika ni Mustafa Mkulo aliyekuwa Waziri wa Fedha, Omary Nundu (Uchukuzi), Dk. Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Profesa Jumanne Maghembe (Kilimo, Chakula na Ushirika), Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara), George Mkuchika (Tamisemi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii) na William Ngeleja (Nishati na Madini).
Kwa mara ya tatu, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri Januari 19, 2014 baada ya kutengua uteuzi wa mawaziri wanne kufuatia ripoti ya Bunge kubaini kuwapo vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, utesaji na udhalilishaji vikidaiwa kutendwa na watekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Ripoti hiyo ya kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilieleza kuwa athari zilizotokana na operesheni hiyo zilisababishwa na wizara nne zilizokuwa zikiongozwa na mawaziri hao.
Waliong’olewa katika sakata hilo ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David.
Chanzo: Mtanzania
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment