Escrow Yawaweka Mawaziri Njiapanda

Hali bado ni tete kwa mawaziri wakati Rais Jakaya Kikwete akiwasiliana na viongozi waandamizi kabla ya kutangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri baada ya kuwa na vikao kadhaa jana na vigogo katika kile kinachoonekana kupata ushauri.
Rais anatarajiwa kutangaza mabadiliko makubwa au madogo wakati wowote, ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano
kuhusu sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow kabla ya chombo hicho cha kutunga sheria kuanza vikao vyake Jumanne ijayo mjini Dodoma.
Sakata hilo, lililohusu takriban Sh306 bilioni zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lilisababisha Anna Tibaijuka kuvuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kubainika kuingiziwa Sh1.6 bilioni na mmiliki wa zamani wa Kampuni ya IPTL iliyo na mkataba na Shirika la Umeme (Tanesco) wa kuizuia nishati hiyo.
Profesa Sospeter Muhongo, ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini anatakiwa aondolewe kwa mujibu wa maazimio ya Bunge na hivyo kuwapo kwa nafasi mbili ambazo Rais atalazimika kuziziba kwa kufanya mabadiliko madogo au makubwa kwenye baraza hilo.
Kwa mujibu wa habari ambazo gazeti hili ilizipata jana kutoka vyanzo mbalimbali, vigogo kadhaa wa Serikali waliitwa Ikulu kwa ajili vikao ambavyo inaaminika kuwa vya kujadili jinsi ya kumaliza sakata hilo, ambalo linafuatiliwa na wananchi na nchi wahisani.
Hata hivyo, wapashaji wetu hawakuweka bayana kuwa vikao hivyo vinahusu kukamilisha kushughulikia sakata hilo lililogusa mawaziri wa sasa na zamani, wanasheria wakuu wa Serikali, watumishi wa umma na viongozi wa kidini.
Habari zaidi zinasema kuwa mkuu huyo wa nchi alikuwa na vikao tangu asubuhi.
Rais anatazamiwa kuondoka Jumapili kwenda nje ya nchi kwa safari za kikazi, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari.
Shinikizo kubwa kwa sasa ni kumwondoa Waziri Muhongo, ambaye Rais Kikwete alisema Desemba 22 mwaka jana kuwa amemuweka kiporo kwa “siku mbili au tatu” kusubiri uchunguzi, lakini mwezi mmoja sasa hakuna uamuzi uliofanywa dhidi ya mtaalamu huyo wa miamba.
Tayari wabunge wa vyama vya upinzani wameshaeleza kuwa watamwondoa kwa nguvu mbunge huyo wa kuteuliwa na Rais iwapo atarejea bungeni Jumanne wakati Mkutano wa 18 wa Bunge utakapoanza mjini Dodoma, wakati mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amesema Bunge halitampa ushirikiano waziri huyo na kwamba atakuwa na kazi ngumu wakati wa Bunge la Bajeti katikati ya mwaka.
Profesa Muhongo anatuhumiwa kutoshughulikia vizuri sakata la escrow na kusababisha Serikali ikose fedha kwa njia ya kodi. Juhudi zake za kujitetea bungeni ziliishia kwa wabunge kutoa vielelezo kadhaa kuthibitisha hoja za kuhusika kwake kwenye sakata hilo.
Credit: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment