Wabunge Wamjia Juu Waziri wa Fedha Saada Mkuya Wataka Afukuzwe Kutokana Kukiuka Katiba

Bunge limeendelea kuwa moto kwa viongozi wakati wabunge wakiwalipua mawaziri, huku wakimtaka Waziri wa Fedha, Saada Mkuya kufukuzwa kutokana na kukiuka Katiba na kumrushia bomu Lazaro Nyalandu kuwa anazunguka nje ya nchi na msichana kwa madai ya kutangaza utalii.
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, pia alikumbana na kadhia hiyo wakati alipodaiwa kuwa anahusika kwenye kila mikataba mibomu, jambo lililosababisha mwanasheria huyo mkuu wa zamani kuingilia kati akitaka “kuheshimiana”.
Wabunge walifanya hivyo jana bungeni mjini Dodoma wakati wakichangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ya mwaka ulioishia Juni 30 mwaka 2014.
Mkuya alijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuonyesha kuwa Serikali ilitumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi mengine, kitendo kinachomaanisha kuwa alivunja Katiba.
Akichangia mjadala huo, mbunge wa viti maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema Bunge limekuwa likitunga sheria na wao kama viongozi lazima waonyeshe mfano wa kufuata sheria.
“Fedha ambazo ziko kwenye ring fence (mfuko maalumu), hazitakiwi kutumika kwa matumizi mengine kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa Katiba, Waziri umevunja Katiba kwa mujibu wa ibara ya 135 na ibara ya 136 ni Tanzania peke yake (Waziri Mkuya) unabaki salama. Hupaswi hata kupewa heshima ya kujiuzulu, unafukuzwa kazi,” alisema Bulaya.
Bulaya, ambaye amekuwa mmoja wa wabunge wachache kutoka chama tawala wanaoihoji Serikali, alisema wizara hiyo imeshindwa kukata fedha kwa ajili ya chai, suti na sambusa na badala yake inakata fedha zilizokuwa ziende kupeleka umeme vijijini.
Alisema fedha hizo zimetengwa ili kuwezesha Watanzania ambao ni masikini kutumia vibatari.
Bulaya alikuwa akizungumzia Sh180.7 bilioni zilizokusanywa kulipia gharama za mradi kutokana na mauzo ya mafuta ili ziweze kupeleka umeme vijijini.
Ripoti inaonyesha kuwa, kati ya fedha hizo, Sh144.2 bilioni ndizo zilizopelekwa kwenye mfuko wa umeme vijijini ikiwa ni pungufu ya Sh36.5 bilioni.
Wakati wa kuhitimisha mjadala wa ripoti hizo, Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Mwigulu Nchemba alikiri kuwa wizara iliyumba katika eneo hilo kutokana na hali ya kifedha ya Serikali.
“Mwaka huu ni hapa tu ambako tuliyumba, (katika) eneo hili la matumizi ya fedha za miradi,” alisema Mwigulu na kuongeza kuwa wizara yake inaandaa utaratibu utakaowezesha makosa hayo kutojirudia.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment