Kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kukojoa kitandani au kujikojolea ni jambo la kawaida. Lakini vijana na watu wazima kujikojolea kitandani mara kwa mara siyo jambo la kawaida katika jamii. Watu wenye tatizo hili hujulikana kama vikojozi.
Kitabu cha afya ya akili kilichotolewa na Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Akili cha Marekani kinasema kwamba kikojozi ni mtu mwenye tatizo la kujikojolea nguoni au kitandani angalau mara mbili ndani ya kipindi cha wiki moja na kwa muda wa miezi mitatu mfululizo akiwa na umri wa miaka mitano au zaidi. Katika tafiti mbili zilizochapishwa mwaka 2003 kuhusu ukubwa wa tatizo la watoto vikojozi, ilibainika kuwa idadi yao ni kubwa katika jamii kufikia kati ya asilimia 14.7 na 20.
Tafiti kadhaa za afya ya jamii zinabainisha kuwa watoto wa kiume hukabiliwa zaidi na tatizo hili kuliko wa kike kwa uwiano wa 2:1.
Pia utafiti mwingine unaonyesha kuwa watoto wa kiume wanakabiliwa na tatizo hili mara tatu zaidi ya watoto wa kike. Katika utafiti uliochapishwa Septemba 2014 katika jarida la kisayansi la IOSR Journal of Dental and Medical Sciences, Dk A.R.C Nwokocha na wenzake wa Chuo Kikuu cha Nigeria walibaini kuwa asilimia 15.82 ya vijana walioko shule za sekondari nchini humo ni vikojozi.
Takwimu nyingine zinaonyesha kwamba katika kila watu wazima 100, mmoja wao ni kikojozi.
Kwa maana hiyo nchi ikiwa na idadi ya watu milioni 50 kama Tanzania, basi idadi ya watu wazima vikojozi inakadiriwa kuwa ni sawa na nusu milioni.
Ingawa tatizo la kujikojolea linaweza kutokea wakati wa mchana, ushahidi mwingi unaonyesha kuwa tatizo hili hutokea mara nyingi zaidi usiku wakati mhusika anapokuwa usingizini.
Hali hii inapomtokea mtoto au mtu mzima, anakuwa hajielewi na ni jambo linalokuwa nje ya uwezo wake katika kujitawala.
Wanasayansi wanatoa sababu nyingi zinazofanya watoto kuwa vikojozi.
Katika utafiti wao Gulnaz Culhal na Nizami Duran wa Chuo Kikuu cha Mustafa Kemal cha nchini Uturuki, walibaini kuwapo kwa uhusiano mkubwa kati ya minyoo aina ya enterobius vermicularis na tatizo la watoto kukojoa kitandani usiku.
Watoto wenye aina hii ya minyoo walikabiliwa na tatizo la kukojoa kitandani kwa asilimia 51.3 na walipotibiwa, tatizo lilipungua hadi kufikia kiasi cha asilimia 28.8.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika jarida la European Journal of General Medicine toleo la 3 (1) la mwaka 2006.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment