Wanafunzi 84 wa programu maalum ya stashahada ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma(udom) waliofanya mgomo na kuandamana kushinikiza kulipwa madai yao, juzi wamepandishwa kizimbani kwa kosa la kukusanyika bila kibali maalum.
Wanafunzi hao ni wa programu maalumu katika masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknohama iliyoanza mwaka jana walifanya mgomo huo juzi na kuandamana kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuwasilisha madai yao.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya hakimu mkazi mwandamizi mfawidhi wa Mkoa wa Dodoma Kabate Richard, mwendesha mashitaka Lopa, aliiambia mahakama kuwa wanafunzi hao walitenda kosa hilo juzi majira ya saa kumi na moja na nusu alfajiri.
Wanafunzi hao wamegawanywa katika makundi manne ya kesi namba 5, 6,7 na 8 ya mwaka 2015 ambapo wanakabiliwa na kosa hilo.
Hakimu huyo baada ya kesi hiyo kusomwa aliwapa dhamana ambapo wanafunzi hao walijidhamini wenyewe kwa shilingi elfu ishirini, ishirini kauli ya maneno.
Wanafunzi hao wapo nje kwa dhamana ambapo kesi zao zimepangwa kusikiliza tarehe 16-19 februari mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment