Wakati CCM ikisubiri Februari kufanya tathmini kuona kama baadhi ya wagombea wake wa urais wametekeleza masharti ya adhabu zao, washindani wao wa Ukawa, Jumanne ijayo watakutana kujadili mambo mbalimbali, ukiwamo mchakato wa kuwapata wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani, imefahamika.
Tangu mwaka huu uanze zimekuwapo pilikapilika nyingi za kisiasa ndani ya vyama vya siasa na Jumanne iliyopita CCM ilifanya kikao cha Kamati Kuu mjini Zanzibar na kutoa maazimio yanayogusia mchakato huo lakini ikasita kutaja ratiba rasmi ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM.
Wakati hali ikiwa hivyo, habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya viongozi wa Ukawa, umoja huo utakutana jijini Dar es Salaam Januari 20, ukiwa na ajenda mbalimbali kuhusu ushirikiano wao, likiwamo suala la kupata wagombea huku vikao vya ndani ya vyama vikitarajiwa mwishoni mwa mwezi huu.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alithibitisha jana kuwapo kwa kikao hicho Jumanne akisema kutakuwa na ajenda nyingine lakini: “Suala la kupata wagombea nalo huenda likajadiliwa. Kuhusu suala la mgombea urais wa Ukawa, linaweza kuwa sehemu ya mazungumzo lakini halipo kwenye ajenda.”
0 comments:
Post a Comment